Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo tarehe 26 Disemba, 2025, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameonesha mfano wa unyenyekevu na ukaribu na wananchi kwa kukutana na kusalimiana na Mzee Abdallah Rashid, mwanzilishi wa Msikiti wa Abdallah Rashid uliopo Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi pia ameswali Swala ya Ijumaa katika msikiti huo, hatua inayotekeleza utaratibu wake wa kawaida wa kusali katika misikiti mbalimbali nchini, kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kijamii na kudumisha mahusiano ya karibu kati ya viongozi na waumini.

Kitendo cha Rais kusalimiana na Mzee Abdallah Rashid, mwanzilishi wa Msikiti wa Abdallah Rashid katika hali ya Heshima na Unyenyekevu kimepokelewa kwa hisia chanya na waumini pamoja na wakazi wa eneo hilo, wakikieleza kama ishara ya kuthamini mchango wa wazee na viongozi wa dini katika kujenga misingi ya imani, maadili na amani katika jamii.
Wananchi waliokuwepo wamepongeza mwenendo wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi, wakisema kuwa unyenyekevu, ushirikiano na ukaribu na wananchi ni sifa muhimu za uongozi bora, unaochangia kuimarisha umoja wa kitaifa na amani ya kudumu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Ziara na ushiriki wa Rais katika ibada za kijamii unaendelea kuakisi dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukuza mshikamano, kuheshimu taasisi za dini na kuendeleza utamaduni wa mazungumzo na amani katika jamii.
Your Comment